WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha St Joseph (SJUIT) Kampasi ya Arusha (kilichofutiwa usajili), waliokuwa chini ya programu ya shahada ya miaka mitano ya ualimu wa sayansi, wametakiwa kusoma ngazi ya cheti au stashahada.
Kama watataka kusoma ngazi ya juu, watapaswa kuomba upya udahili.
Aidha, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imesema wanafunzi waliokuwa wakipata mkopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), mikopo yao pia imesimamishwa.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Simon Msanjila alitoa agizo hilo jana kupitia taaarifa kwa vyombo vya habari.
Profesa Msanjila alisema hatua hiyo, inatokana na kubainika kwamba wanafunzi hao hawastahili kusoma shahada na pia hawakustahili kupewa mkopo.
“Tunawafahamisha wanafunzi wa SJUIT waliokuwa kwenye programu ya miaka mitano kwamba watatakiwa kuishia daraja la cheti na stashahada... Kama wanafunzi hao watataka kuendelea na masomo ya juu, watatakiwa kuomba upya,” ilisema taarifa hiyo.
Februari 25, mwaka huu, Wizara kupitia Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) baada ya kujiridhisha kuwa Kampasi ya Arusha ya Chuo Kikuu cha Mt. Joseph Tanzania imepoteza sifa na vigezo vya kuendelea kutoa elimu ya chuo kikuu, ilifuta kibali cha kuanzishwa kwake.
Iliidhinisha uhamisho wa wanafunzi wote, waliokuwa wanasoma katika Kampasi hiyo ya Arusha kwa gharama za Chuo Kikuu cha SJUIT.
Aidha, ilifuta udahili wa wanafunzi wapya katika programu ya shahada ya miaka mitano ya ualimu wa sayansi.
Ilielekeza wanafunzi waliokuwa wakiendelea na masomo katika programu hiyo, wahamishiwe katika Kampasi ya Luguruni, Dar es Salaam.
TCU ilielekeza kwamba wanafunzi watalazimika kwanza kuhitimu katika ngazi ya Stashada, kama ilivyokuwa imeidhinishwa na Tume hapo awali.
Wanafunzi waliohamishiwa kwenye vyuo mbalimbali, waendelee na masomo.
Taarifa hiyo ilisema wakati wa mchakato wa uhamisho, wanafunzi wote walihakikiwa kubaini kama wanakidhi vigezo vya kusoma kwenye ngazi hiyo.
Wanafunzi wote waliokuwa wakisoma programu hiyo ya miaka mitano, walihamishiwa kwenye Kampasi ya Luguruni, jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo kutokana na mchakato wa uhakiki, baadhi ya wanafunzi walikutwa hawana sifa za kujiunga na mafunzo hayo ya ualimu.
Wale waliobainika kuwa na sifa, walitaarifiwa kuendelea na masomo kwenye kampasi hiyo ya Luguruni.Wanafunzi katika kundi hili waliobainika kuwa na vigezo, walitaarifiwa kuendelea na masomo katika Kampasi ya Luguruni.
"Maana ya kuwa na vigezo vya ufaulu tunavyovizungumzia hapa ni kwamba wanafunzi husika wamefaulu katika masomo lengwa yanayowawezesha kusoma Cheti cha Ualimu Daraja “A” ambacho ni kigezo cha kwanza kwa mujibu wa mtaala wa programu hiyo."
0 comments:
Post a Comment