Kocha wa timu ya taifa ya soka ya Cameroon Volke Finke amefutwa kazi.
Uamuzi huo ulifanywa na kamati kuu tendaji ya Shirikisho la Soka la Cameroon (Fecafoot) Ijumaa.
Finke, 67, ambaye ni raia wa Ujerumani, amekuwa akinoa timu hiyo tangu Mei 2013 lakini chini ya uongozi wake, timu hiyo imeandikisha msururu wa matokeo mabaya hasa katika fainali za Kombe la Dunia 2014 na fainali za Kombe la Taifa Bingwa Afrika 2015.
Fecafoot walitangaza kupitia akaunti yao kwenye Twitter kwamba Alexandre Belinga ameteuliwa kaimu kocha mkuu wa timu na atasaidiwa na Djonkep Bonaventure.
Wawili hao sasa huenda wakawa ndio watakaoiandaa Cameroon kwa mechi mbili za kufuzu kwa Kombe la Dunia 2018 dhidi ya Niger Novemba 13 na 17.
Cameroon wakati mmoja walijulikana kwa ubabe wao wa soka Afrika lakini kwa miaka mitano sasa wametatizika. Finke hakuweza kubadilisha mambo.
Katika Kombe la Dunia nchini Brazil, timu hiyo chini ya Finke ilishinda mechi zote tatu na baadhi ya wachezaji wake waliadhibiwa kwa utovu wa nidhamu. Alex Song alionyeshwa kadi nyekundu nao wenzake Benoit Assou-Ekotto na Benjamin Moukandjo wakapigana uwanjani.
Cameroon walionekana kujikwamua kutoka kwa masaibu hayo walipofuzu kwa fainali za Kombe la Taifa Bingwa Afrika nchini Equatorial Guinea bila kushindwa lakini walibanduliwa nje hatua ya makundi kwenye fainali hizo.
SOURCE:BBC SWAHILI
0 comments:
Post a Comment