RAISI MAGUFULI AONGELEA SAKATA LA MAALIM SEIF KUKATAA MKONO WA RAISI SHEIN

Rais John Magufuli amemshangaa Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kwa kuidhinisha fedha za matibabu ya mpinzani wake wa kisiasa, Maalim Seif Sharif Hamad wakati alikataa kumpa mkono wa salamu walipokutana kwenye mazishi wiki mbili zilizopita. 

“Mtu mmekutana kwenye msiba, mahali kwenye majonzi, mnamsindikiza marehemu. Kwa unyenyekevu wako Dk Dhein ukatoa mkono wako kumsalimia mtu fulani. Huyu mtu akakatalia mikono yake na bado asubuhi yake ukasaini fomu zake za kwenda kutibiwa nje ya nchi?” alisema Magufuli. 

“Haya ni mapenzi makubwa sana. Amekataa mkono wako. Huyohuyo akiugua unampeleka hospitali. Akitaka kusafiri nje, unasaini na unampa na fedha na posho za kwenda nje. Mimi nisingeweza.” 

Rais ametoa kauli hiyo jana wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika kisiwani Unguja ambako amekwenda kushukuru wananchi kwa kumchagua kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita. 

Visiwani Zanzibar, uchaguzi wa Rais, wawakilishi na madiwani uliingia dosari siku ya mwisho ya kutangaza matokeo. Mwenyekiti wa Tume ya Ucha- guzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha alifuta matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, wawakilishi na madiwani Oktoba 28 mwaka jana, siku ambayo alitarajiwa kutangaza mshindi wa mbio za urais. 

Alifuta wakati matokeo ya majimbo 31 yakiwa yameshatangazwa na kubakia tisa ambayo yalishahakikiwa na kusubiri kutangazwa huku baadhi ya washindi wa viti vya uwakilishi wakiwa wameshatangazwa na kupewa vyeti. 

Jecha alisema kulikuwa na ukiukwaji wa sheria na kanuni za uchaguzi na kutangaza uchaguzi mpya Machi 20, lakini chama kikuu cha upinzani visiwani humo, CUF kikasusia na tangu wakati huo uhusiano baina ya wafuasi wa vyama hivyo umeharibika. 

Uhasama huo ulifikia kiwango cha juu wakati Maalim Seif alipokataa kumpa mkono Dk Shein walipokutana kwenye mazishi ya Rais wa Pili wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi kitendo kilichomfanya Rais Magufuli aeleze yake ya moyoni jana. 

Akishangiliwa na wananchi, ambao wengi walivalia fulana za rangi za njano na kijani ambazo hutumiwa na CCM, Rais Magufuli alisema Dk Shein ni mpole na kama angekuwa na moyo kama wake, hali ingekuwa tofauti baada ya kufanyiwa kitendo hicho cha Maalim Seif. 

“Niutoe mkono wangu, uukatae halafu kesho niende ofisini kukusainia wewe (akaongea kilugha). Ndiyo maana nasema wewe ni special. Nafikiri wanapotoka malaika wewe ndiyo unafuata. Kama mtu anaukataa mkono wako, na wewe kataa kufanya mambo yake, ajifunze kwamba na wewe mkono wako una thamani.” 

Alisema anaomba Mungu amsaidie kumpa angalau nusu ya moyo wa Dk Shein na kuomba Mungu ampe Dk Shein nusu ya roho na mawazo yake ili Zanzibar iende bila kelele za aina yoyote. 

“Jana nilikwambia angalau uongeze kaukali kidogo. Umefanya mambo makubwa sana katika nchi hii. Tulishazungumza na wewe umezungumza kwamba kwa mujibu wa Katiba, uchaguzi umekwisha, ukisharudiwa umekwisha. Utarudiwa tena mwaka 2020, wazunguke waimbe lakini wewe ndiye rais,” alisema. 

Magufuli alisema upendo na unyenyekevu alionao Dk Shein ni wa hali ya juu kwani licha ya mikikimikiki aliyoipata kutoka kwa wapinzani, ameendelea kuwaingiza katika Serikali yake, jambo ambalo yeye hawezi kulifanya. 

“Mimi nilipata ushindi kwa asilimia 58, lakini hakuna mtu kutoka chama kingine atakayekanyaga mguu kwenye Serikali yangu. 

"Mzee huyu ana moyo wa tofauti, namuomba Mungu apate hata robo ya moyo wangu maana amekuwa mpole mno,” alisema Dk Magufuli. 

Rais Magufuli alisema licha ya maendeleo yaliyopo, bado wapo Wazanzibari (hakuwataja majina) wanaokwenda nje ya nchi na kuwazuia wageni na watalii kuacha kutembelea visiwa hivyo. 

“Mwenyeji anakuja na kuwaambia wageni wasije hapa na wao wamempuuza. Bado wageni wanakuja. Ukigombea mwaka wa kwanza ukashindwa, mwingine ukashindwa, mwingine ukashindwa, huwezi kujifunza hata kwenda kuuza nyanya sokoni kwamba biashara hii imekataa kwako,” alisema na kuongeza:

“Kwani hakuna wengine ambao wanakuja? Kuna mtu alitegemea kwamba nitakuwa Rais, hata kuota.Lakini nimekuwa waziri kwa miaka 20 sikujaribu hata siku moja kugombea (urais). 

“Unajua vyeo hivi vinaletwa na Mungu, hata uzunguke namna gani, hata ufuge ndevu namna gani hata unyoe. Kama kasema hapana ni hapana tu, ndiyo maana nasema watu, ni shetani kama sivyo, basi ana moyo wa kishetani na mtu anayefarakanisha mke na mume kwa itikadi za vyama vyao pia ni shetani. 

0 comments:

Post a Comment