Afisa Mafunzo wa TMF, Raziah Mawanga akizungumza jinsi TMF inawasaidia waandishi wa habari ili waweze kufanya kazi zao kwa weledi. Kushoto ni Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri na Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Deodatus Balile. Kulia ni Mwenyekiti wa MISATAN, Simon Berege na Ofisa Miradi katika Kitengo cha Mawasiliano na Tehama UNESCO, Nancy Kaizelege
Mwaka huu maadhimisho hayo yatafanyika jijini Mwanza na kuhudhuriwa na viongozi wengine wa ndani na nje ya nchi ambapo kaulimbiu ni KUPATA TAARIFA NI HAKI YAKO YA MSINGI.
Akizungumzia sherehe hizo katika mkutano na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa MISATAN, Simon Berege amesema sherehe za mwaka huu zinatarajia kuwa na wageni zaidi ya 250 akiwepo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Alvaro Rodriguez na Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Zulmira Rodrigues.
Aidha Berege amesema kuwa siku ya uhuru wa vyombo vya habari kwa mwaka huu itafanyika kwa siku mbili, Mei, 2 kutakuwa na kongamano ambalo litatumika kujadili hali ya uhuru wa vyombo vya habari nchini na Mei, 3 ndiyo itakuwa siku husika ya maadhimisho.
“Kikawaida huwa kuna mambo tunafanya katika siku hiyo, tutawakumbuka waandishi wa habari waliopoteza maisha kazini, tutawakumbuka waandishi wa habari maveterani na waandishi wa habari waliopatwa na matatizo wakiwa kazini … kwa mwaka huu tutakuwa na mambo ya kipekee tofauti na miaka iliyopita,” amesema Berege.
Pia ameongeza kuwa watapitia sheria zinazohusu uhuru wa vyombo vya habari kama Cyber Crime Act 2015 na Sheria ya Takwimu 2015 pia kuipitia miswada ya huduma ya vyombo vya habari na uhuru wa kupata taarifa.
0 comments:
Post a Comment